Thursday, November 26, 2009
SIPENDI JINA LA OBAMA
RAIS WA MAREKANI BARACK OBAMA
MDOGO WAKE OBAMA,Mark Ndesandjo
Mark Ndesandjo ni mdogo wa Rais Barack Obama...anasema hakupenda kabisa kutumia jina la Obama wala kuuenzi utamaduni aliouita wa Kiafrika mpaka baada ya kaka yake kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Kaka huyo wa Rais Obama alizaliwa mwaka 1966 na mama yake ni raia wa Marekani mwenye asili ya Kiyahudi.
Mama huyo anaitwa Rurh Nidesand ambaye aliolewa na Barack Hussein Obama mara baada ya baba huyo kuachana na mama yake Rais Obama, Stanley Ann Dunham ambaye naye pia alikuwa raia wa Marekani.
Wiki hii Ndesandjo anayeishi nchini China ambako Rais Obama alikuwa ziarani, alitawala katika vyombo vya habari vya kimataifa baada ya kuzindua kitabu chake kikielezea ukatili wa baba yake mzazi.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu uzinduzi wa kitabu hicho alichokiita ‘Nairobi to Shenzhen’ kwenye mji wa Guangzhou nchini China, Ndesandjo aliweka wazi kwamba hakuwa akijisikia fahari kutumia jina la Obama na ilimchukua muda mrefu sana kuja kuona fahari kutumia jina hilo.
"Katika maisha yangu sikutaka kuhusishwa na jambo lolote linalohusiana na baba yangu pamoja na baadhi ya tabia za utamaduni wa Kiafrika, nisingependa hata kutumia jina la Obama," anasema Ndesandjo.
Sababu kubwa ya kufikia uamuzi huo ni tabia ya baba yake kumpiga mama yake na hata yeye kupata kipigo ambacho anasema kilimfanya kumchukia sana baba huyo.
Haijulikani kama uzinduzi wa kitabu hicho ulilenga pia kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake ambayo imeanza wiki hii duniani kote.
Kwa muda mrefu ndugu huyo wa Rais Obama amekuwa akitumia jina la Ndesadjo ( linatamkwa de-SANZ-jo) ambalo ni jina la mume wa pili wa mama yake na hata katika utambulisho wa kitabu hicho, hakutumia jina la Obama kama kampuni nyingi za uchapishaji zilivyoshauri.
Katika kitabu hicho, Ndesandjo anasema baba yake alikuwa katili na asiyekuwa na mfano wa kuigwa. Ukatili huo ulimhuzunisha na alihisi kuwa hakuwa anapendwa katika familia hiyo.
Alisema kuwa mama yake alipigwa sana na baba yao huyo kitu ambacho kilimfanya naye kuumia kutokana na kipigo hicho cha mama na wakati mwingine alipigwa yeye hali iliyomfanya kuiona familia hiyo ya Obama kuwa yenye uovu na isiyofaa na kulalamika kwanini amezaliwa katika ukoo wa Obama.
“Baba yangu alimpiga mama yangu na alinipiga na mimi,” anasema mdogo huyo wa Rais Obama katika mahojiano na Shirika la Habari la Associated Press mjini Beijing na kuongeza kuwa hali hiyo anaikumbuka wakati akiwa mdogo.
“Sikuwa na kosa…sijui kama kweli nilikuwa na kosa mpaka anipige lakini nimeshamsamehe kwa yote aliyonitendea,” aliongeza.
"Baba alifanikisha mambo aliyoyataka na hasa kwa kutumia uwezo wake wa akili, alifanikisha kusoma Harvard na kuishi maisha ya juu katika jamii ya Marekani.
“Lakini kuna kitu kilimtokea, nadhani ni mchanganyiko wa ulevi, kutokufikia malengo yake na labda kutokujitambua yeye mwenyewe ambavyo vilichangia yeye kuwa mkatili nyumbani.
“Hata mama yangu aliniambia kuwa baba alikuwa na akili sana lakini alishindwa kufaulu katika maisha yake binafsi,” anasema Ndesandjo.
Pamoja na kusikitishwa na kumchukia baba yake kwa mateso makubwa aliyompa hali iliyosababisha kuichukia jamii ya Obama, kwa sasa baada ya ushindi wa kaka yake alioupata katika uchaguzi mkuu wa mwaka amebadili mwelekeo.
“Najivunia sana kuwa miongoni mwa familia ya Obama, namshukuru Mungu kwa kuwa raia wa Kenya nitokanaye na Barack Hussein Obama, Mungu aibariki familia hii,” anasema Ndesandjo katika kitabu chake kilichozinduliwa katika mji wa Guangzhou.
Baba huyo alioa wanawake watatu, wa kwanza akiwa ni raia wa Kenya na walifanikiwa kupata watoto wanne.
Mke wa pili alikuwa mama yake Rais Obama ambaye walikutana alipokuwa masomoni Marekani na hatimaye walioana na kufanikiwa kuwa na mtoto mmoja ambaye ni Rais Obama.
Mwaka 1964 waliachana na mama yake Obama na kumuoa mama yake Ndesandjo mpaka Barack Hussein Obama anafariki mwaka 1982 katika ajali ya gari, alikuwa na mke huyo.
Wadadisi wa mambo wanasema Rais Obama ana bahati kubwa na mvuto wa kipekee kutokana na kuwavutia watu wa kila rangi. Bahati hiyo imeonekana pale alipowawezesha waliokorofishana naye kuwa pamoja, waliochukizana walipatana na ndio maana hata mdogo wake aliyejitenga naye alikuwa pamoja naye baada ya ushindi wake katika uchaguzi.
Anasema kwa kipindi kirefu sana alikaa kimya bila kusema kwa sababu umaarufu wa familia hiyo ulitaka kuisha au kufikia ukingoni, lakini kwa bahati nzuri ikaokolewa na kaka yake yaani Rais Barack Obama alivyochaguliwa kuwa Seneta wa Illinois na baadaye kuwa Rais wa nchi hiyo kubwa kiuchumi na kijeshi duniani.
Kukutana Ndesandjo na Obama Ndesandjo anasema wakati aliposikia kuwa kaka yake anagombea urais nchini Marekani mwaka jana, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi aliamua kwenda Texas nchini Marekani kwa kutumia fedha alizokuwa akidunduliza kwa ajili ya kununua kinanda, ili aweze kumuona kaka yake huyo kwa mara ya kwanza.
“Cha kwanza kabisa nilimkumbatia, akaniangalia sharubu na akasema ni vitu gani hivi vikubwa hapa? Nikamwambia hizi ni sharubu, kisha akasema tena una nywele ndogo zaidi ya nilivyokuona mara ya kwanza, nikamwambia unapenda kubwa, akasema nisingeweza kuzigharamia,” alisema Ndesandjo.
Alihamia nchini China akitokea Marekani baada ya kupoteza kazi yake katika shirika moja la mawasiliano kulikotokana na mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001.
Mwaka uliofuata alihamia China na kuwa mwalimu wa somo la Kiingereza na kinanda. Pia alianza kujifunza Kichina na kusaidia wasiojiweza na yatima. Katika kipindi hicho chote alifanikiwa kuandaa kitabu hicho kilichobeba sifa na wasifu wa baba yake.
Akiwa China Ndesandjo ameishi kwa takribani miaka saba sasa na katika kipindi hicho amefanikiwa kuoa mke ambaye ni raia wa China ambao kwa pamoja wanaishi katika mji wa Shenzhen uliopakana na Hong Kong.
Kwa upande wake Rais Obama anasema amefurahishwa kukutana na kaka yake na amejisikia furaha sana kutokana na kuonana na mdogo wake huyo.
Hata hivyo Rais Obama anasema hana uhakika na tuhuma za mdogo wake kwa kuwa kila mtu anatoa wasifu wa mtu kutokana uzoefu na namna amjuavyo japo anakiri kuwa baba yao alikuwa mlevi kupindukia.
Rais huyo wa Marekani anasema mtazamo wake unatokana na maisha aliyokulia ambayo mama yake mzazi hakuwa na rekodi ya kuonewa sana kama ilivyokuwa kwa mama yake Ndesandjo.
Anasema pia hana kumbukumbu sahihi za baba yake huyo kwa kuwa alitengana naye alipokuwa na miaka miwili tofauti na Ndesandjo ambaye alikuzwa nchini Kenya chini ya malezi ya baba yao huyo.
Amesema alifurahishwa sana na ndugu yake huyo kwa kuhudhuria katika sherehe za kumwapisha kuwa Rais wa Marekani mwanzoni mwa mwaka huu.
"Nilifurahi sana kufika kwake lakini pia nilisikitishwa sana kwa kushindwa kuonana na yeye uso kwa uso,” alisema Obama katika mahojiano na Shirika la Habari la Ufaransa AFP. Rais Obama alifanikiwa kumuona baba yake mara ya mwisho akiwa na miaka 10.
Aliandika kitabu chake kiitwacho ‘Dreams from my father’ ambacho ndani alimwelezea baba yake kuwa alipewa ‘zawadi’ lakini alikuwa mlevi asiyejali familia.
www.haki-hakingowi.blogspot.com"
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment